JITAFUTE
10th March
2018
By Pastor Sam Gripper
“Kwakuwa mtu atakaye
kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwaajili
yangu ndiye atakaye isalimisha. Kwakuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote,
kama akajiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”
LUKA 9:24-25
Kikubwa
nitakacho andika siku ya leo kwa msaada wa Mungu, ni sababu inayoweza kumfanya mtu
kujikuta katika point ya kujiangamiza na kujipoteza mwenyewe na namna ambavyo
anaweza akajitafuta ili kurudi katika mpango wa Mungu.
Jambo la
kwanza na la msingi ambalo nataka kulizungumzia hapa ni kwamba, kitu chochote
katika maisha yako ambacho umekipa nafasi ya kukutafsiri, kitu hicho kina
nafasi kubwa sana ya kuelezea uelekeo wako. Mara nyingi tumeviangalia vitu
ambavyo havijabeba maana ya jinsi tulivyo na tukahisi ndiyo vitu vinavyotafsiri
namna tulivyo, tukaviacha vitutafsiri, na vikatupeleka katika point ya kujipoteza huku
tukidhani kuwa tumejikamilisha katika hivyo.
“Msisumbuke, basi,
mkisema, Tule nini? Au tunywe nini? Au tuvae nini? Kwa maana hayo yote mataifa
huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
Basi utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”
MATHAYO 6:31-33
Mahitaji ya
kimwili, ni moja kati ya vitu ambavyo tumehisi vinatafsiri jinsi tulivyo na
tukavipa nafasi ya pekee sana, na mwishowe vinatupeleka katika kujipoteza.
Katika kitabu cha Mathayo hapo juu, Yesu anataka tupate ufahamu wa kujua ni
nini kinacho tutofautisha na mataifa (watu wasiomjua Mungu/kwa mazingira ya
andiko hili, ni watu wasio Waisrael).
Kila
mwanadamu, awe ameokoka au hajaokoka, yapo mambo anayoyahitaji. Utofauti wetu
kama wana wa Mungu na watu ambao bado hawajamjua Mungu, unatakiwa kuwa katika
namna tunavyoyatazama mahitaji yetu (mtazamo wetu kwa mahitaji yetu) na namna
tunavyopiga hatua za kuyafikia.
Watu
wasioijua kanuni ya Ufalme, wanatafuta mahitaji, lakini tunaoijua na kuiishi
kanuni ya Ufalme, tunautafuta ufalme, maana hatuenendi kwa jinsi ya kuona
lakini kwa jinsi ya Imani, na jambo kuu tunaloamini ni kwamba Mungu anajua yote
tunayoyahitaji na anaweza kutupatia kwa ukamilifu, hivyo hatutendi wala
kuenenda kwa hofu.
Mara zote
tunajipoteza wenyewe ndani ya vitu ambavyo tumevitengeneza kwa mikono yetu
wenyewe. Vitu vinavyozaa hofu na mashaka ya kujiona kila siku kuwa
hatujakamilishwa na tunahitaji kujikamilisha kwa jitihada zetu binafsi.
Katika
Mwanzo sura ya 11, Mungu aliweza kuona jaribio la watu wale kujifanyia mnara ni
jaribio la kuwapeleka upotevuni, kwasababu ni jambo lililokuwa matokeo ya
jitihada zao za kutaka kujijengea namna ya kuwatafsiri na kuwatambulisha kwa
mafikio yao. Na jambo hili, likatafsiri ueleke wao.
Mahali
ambapo tunauhakika wa kutojipoteza ndani ya mambo tunayoyahitaji, sio mahali
tunapohitaji kujipatia uhuru wa kushughulika na mambo hayo kwa nguvu zetu
binafsi, lakini ni mahali ambapo tutatafuta na kuuona ukamilifu wa mambo
tunayoyahitaji yakitokana na nguvu zetu za kuutafuta kwanza Ufalme wa Mungu.
Kuwa na
nguvu ya kumtafuta Mungu badala ya mahitaji, haimaanishi tusijihusishe na
shughuli yoyote ya uzalishaji na tuanze kushinda makanisani. Lakini inamaana
kuwa katika kila tulifanyalo, lazima tuwe na uhakika kuwa tupo na tunaishi
ndani ya kanuni za Ufalme. Adamu ndani ya bustani ya Edeni, alikamilishwa
katika kila kitu kwakuwa kila alichokihitaji na kukifanya, alikipata na kukifanya
akiwa ndani ya uwepo wa Mungu.
Sio
unayoyahitaji ndiyo hutafsiri wewe ni nani, lakini ni vile ulivyojiwekeza
katika Ufalme wa Mungu ndiyo hukutafsiri wewe ni nani.
“Kwa sababu hiyo
nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini, wala miili yenu
mvae nini. Maisha je, si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?”
MATHAYO 6:25
“Akawaambia, Angalieni,
jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake
alivyonavyo.”
LUKA 12:15
#Jitafute
© Pastor Sam Gripper
TAG PENUEL LUHANGA/TOTAL
TRANSFORMATION
grippersamuel@gmail.com
No comments:
Post a Comment