KUISHINDA
HATIA
21ST
JANUARY 2018
Pastor Sam
Gripper
UTANGULIZI
Kupitia
utafiti wangu mdogo na usio rasmi sana, lipo jambo niligundua kuhusu hatia.
Hatia, ni jambo pekee ambalo linaweza likaishi na mtu kwa muda mrefu sana hata
kama kosa ambalo huyo mtu alilifanya lilifanyika mara moja tuu tena miaka
kadhaa iliyopita.
Hii
inanipeleka katika point ambayo natakiwa kuamini kuwa sababu pekee ya watu
wengi kuhisi hawana nguvu wala uwezo wa kuishi maisha matakatifu, au kujiona
wao ni wa dhambi na hakuna point Mungu anaweza akawakubali, si kwasababu ya
dhambi walizozitenda lakini ni kwasababu ya hatia ambazo dhambi walizozitenda
zinaiazalisha ndani yao na kutafsiri kila hatua ya maisha yao.
Iko
point ambayo dhambi na hatia hukutana. Kwa tafsiri rahisi, dhambi ni kukosea
shabaha, au kutenda chini ya kiwango/viwango vilivyokusudiwa. Hatia huzaliwa
pale ambapo mtu hutakiwa kuwajibika kulingana na kukosea kwake shabaha au
kuishi na kutenda chini ya viwango vilivyo kusudiwa.
Hatia
ni hisia mbaya sana na huambatana na maumivu makubwa mno ambayo kimsingi huweza
hata kugharimu maisha ya mtu. Kama hatutajua namna ya kushughulika na hatia
zinazozalishwa ndani yetu kwa sababu ya makosa mbalimbali, tutakuwa tupo mahali
pa hatari sana.
Kila
mtu huwa kuna mahali anakosea, na kutokana na kosa husika hukumbana na hali hii
ya kushambuliwa na hatia. Si ajabu hata baadhi watu waliookoka wakawa wanapitia
hali hii pia.
Somo
hili kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ni hatua ya kutufungua fahamu zetu juu ya
kushughulika na hatia zetu na kutufanya tuuishi na kuufurahia uhuru ndani ya
Kristo
MAANA YA HATIA
Nikiwa
nipo chekechea zamani sana, niliwahi ku experience namna hatia inavyotesa na
hata ninapoongozwa kukuletea somo hili, naelewa hasa ni nini nakizungumzia na
kwa upana gani natakiwa nikizungumzie. Naweza kusema kama mtoto, kwangu mimi
ndiyo ilikuwa mara ya kwanza nayahisi maumivu haya ya hatia.
Siku
moja nikiwa na rafiki zangu tukiwa njiani kutoka shuleni, nilijikuta natamani
sana bagia. Na kwakuwa nilikuwa tayari nimeitumia hela yangu yote wakati wa
mapumziko, sikuweza kununua. Nilipofika nyumbani, nilikuta mama ndiyo kwanza
anawasha moto ili apike chakula cha mchana.
Kwakuwa
nilikuwa naelewa wapi mama huwa anaweka hela, niliingia moja kwa moja hadi
chumbani kwake na kuchukua shilingi hamsini kisha nikarudi shuleni (kwakuwa
hapakuwa mbali sana na nyumbani), kuzifuata zile bagia. Nilinunua za kutosha,
na nikawagawia baadhi ya rafiki zangu pia.
Niliporudi
nyumbani, nilikuta chakula tayari kipo mezani na mama na kaka yangu tuliyefuatana
kuzaliwa wameshaanza kula muda mchache tuu. Nilipokata tonge la ugali na
kutoweza katika ile mboga, nilihisi inamapungufu makubwa sana, ingawa sikuwa
najua sana kuhusu mapishi lakini niliweza kuhisi. Na kikawaida, nilikuwa
mwepesi sana kulalamika pale kinapopikwa chakula nisichokipenda au pale chakula
kinapopikwa katika namna nisiyoipenda.
Dakika
hii, kabla sijaanza kulalamika, nikakuta mama ndiyo anakuwa wa kwanza kuongea.
Hakuongea maneno mengi, yalikuwa machache lakini yaliuchoma moyo wangu kwa
hatia kuu. “Mmeona, tunakula mboga ambayo haina kitunguu kwasababu mmoja wenu
aliingia chumbani na akachukua hela ambayo ilitakiwa tununulie kitunguu. Sasa
ametufanya tule mboga isiyo na kitunguu.”
Naamini
mama alijua kuwa nimechukua ile hela, na hakukosa hela ya kununulia kitunguu,
lakini alitaka anifundishe jambo kubwa. Sikuwa na nguvu ya kuadmit kuwa ni
mimi, lakini niliumia kiasi kilichofanya nijione nimekuwa na hatia. Nikadhamiria, kesho yake
nitakapopewa hela ya shule, nitairudisha mahali nilipoichukua ile nyingine.
Nilijikuta naumia sana. Nikafanya hivyo.
Hatia inaelezewa
Hatia ni hisia inayokuleta katika point ya
kuwajibika kutokana na ukosefu au kosa ulilolitenda. Hisia hii inaweza kutokana
na kufanya jambo ambalo ni katazo au kushindwa kufanya jambo lililokuwa
likihitajika lifanyike.
Na
kimsingi ni kwamba, tunakutana na kuingia katika hatia kwasababu tumezungukwa
na sheria na taratibu nyingi ambazo zipo kutuongoza katika njia njema ya
maadili. Tunaposhindwa kuzitimiza, au tunaposhindwa kuzifuata, tunajikuta
katika point ambayo tunatakiwa tuwajibike kwa yale tuliyotenda au tuliyoshindwa
kuyatenda.
Hatia,
ni hisia pekee ambayo itakutesa hata kama wengine hawajui kosa au dhambi
uliyoifanya. Na ndio maana tupo na watu wengi makanisani, mashuleni na maeneo
mbalimbali ya shughuli za kila siku, ambao kutoka kwao, tunaweza tusione makosa
au mapungufu yoyote na tukahisi ni wakamilifu sana, lakini ndani yao panaweza
kuwa na mzigo huu wa hatia juu ya mambo flani flani waliyowahi kuyafanya au
wanayoyafanya.
Na
kwasababu hatia ni mzigo unaoambatana na maumivu, kujichukia, kujilaumu nk.
Wengi mara baada ya kukosa hujaribu sana kuficha dhambi au makosa yao huku
wakiendelea kujichukia au hulaumu hali au mazingira ambayo yaliwafanya kuingia
katika aina hizo za makosa. Hivyo kadri wanavyolaumu wengine au mazingira au
kadri wanavyojitahidi sana kuficha makosa yao, wanahisi mzigo wa hatia ndani
yao hupungua, lakini kimsingi, sio kweli.
“Adamu
akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja name ndiye aliyenipa matunda ya mti
huo nikala.”
MWANZO 3:12
Hii
ni tabia ya wanadamu wote. Ni wachache sana ambao katika kukosa, watakubali
kuuvaa wajibu wa kukubali kuwa wao ndio chanzo cha makosa, mapungufu na
maharibifu. Lakini wengi, watasingizia mazingira, watasingizia au hali zozote
ili kuukwepa mzigo huu wa hatia ndani yao, lakini kimsingi haukwepeki katika
namna hiyo.
MTU, DHAMIRI NA ROHO MTAKATIFU
Asilimia
kubwa ya watu ambao kutoka kwao mataifa (watu ambao bado hawajamjua Mungu)
walitegemea kuwa watapata msaada wa kiroho ndiyo watu ambao wanaishi maisha ya
kushindwa (defeated life) na kushtakiwa kila mara kwa sababu ya yale waliyowahi
kuyatenda au wanayoyatenda.
Kwa
sehemu tuu, niliwahi kupata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya vijana wenzangu
kadhaa ambao walinitafuta kibinafsi kabisa, (ni vijana wanaotumika kanisani) kunielezea
ni kwa kiasi gani wamekuwa addicted na baadhi ya matendo au tabia zisizo faa na
hawaoni namna ya kutoka katika vifungo hivyo.
Katika hali ya utulivu kabisa ya kuzungumza
nao juu ya hali hizo (maana na mimi pia nimewahi kupitia), nikagundua, asilimia
kubwa (sio wote) ya watu ambao wanadhani wanateswa na aina flani ya tabia
mbaya, dhambi au vifungo, katika namna halisi kabisa, huwa hawateswi na hizo
dhambi lakini huteswa na mashtaka ya hizo dhambi.
Wengi
ambao nimezungumza nao, huwa ninapenda kuwauliza hili swali, “Mara baada ya
kujikuta umefanya hiyo dhambi, ulitubu?” Karibia wote hujibu ndiyo, kitu
ambacho hunipeleka katika swali lingine, “Kama ni kweli ulitubu tena kwa
kumaanisha, ni kwanini bado uendelee kushtakiwa na kushikiliwa katika kifungo
ambacho tunaamini toba imekutoa?” Na kimsingi, huwa wanakosa majibu na
kuniambia kila mara wanajikuta wana mzigo wa ile dhambi, na inafika point hadi
wanajichukia.
Hivyo
nataka tupate picha kuwa dhambi huweza kufanyika mara moja tuu, lakini hatia
inayozalishwa kutokana na hiyo dhambi huweza kudumu milele kama tuu hatujajua
namna Roho Mtakatifu anavyotenda
katika Dhamiri zetu ili kutufunulia
Upendo, Rehema na Neema ya Mungu kwetu.
Dhamiri
Kila
mwanadamu anayo dhamiri. Na dhamiri ni moja kati ya vitu vinavyo akisi sura ya
Mungu kwa mwanadamu, vingine ni utashi (uwezo wa kufanya machaguo na maamuzi),
kuunda/kuumba na mengine mengi.
Dhamiri,
ni uwezo au tabia ya asili (inayotokana na Mungu mwenyewe) inayotawala kiwango
cha utakatifu wa mtu ili awe mtakatifu kama vile Mungu alivyo mtakatifu.
Unaweza kuwa huijui dini yoyote, huna maadili yoyote ya kijamii, lakini kuna
kitu ukifanya, ndani ya moyo wako utaisikia hukumu kuwa jambo ulilolifanya
halikuwa sahihi. Ndivyo ambavyo dhamiri hufanya kazi.
Hivyo,
wakati utashi unampa uhuru mwanadamu juu ya kufanya machaguo na maamuzi
mbalimbali, dhamiri inamuwajibisha au kumshuhudia wanadamu juu ya maamuzi
aliyoyafanya kama ni halali ama si halali.
“Kwa kuwa
wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye
sheria, watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu, sio wale waisikiao sgeria walio
wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.
Kwa maana
watu wa mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati,
hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi
ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao,
dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao wenyewe kwa yenyewe, yakiwashtaki au
kuwatetea.”
WARUMI 2:12-15
Hivyo
katika maandiko haya, Paul anajaribu kuonesha kuwa hapana upendeleo mbele za
Mungu, kila mtu atahukumiwa kulingana na matendo yake. Wayahudi kwakuwa
walikuwa na sheria/Torati walitakiwa kuhukumiwa kwa hiyo, na watu wa mataifa
ambao hawakupewa kuongozwa na torati, watahukumiwa kwa dhamiri zao.
Hivyo
Mungu alidhamiria kuwa dhamiri iwe ni alama au jambo litakalo muongoza
mwanadamu katika utakatifu wote wa Mungu. Ndio maana tunapokosea, dhamiri zetu
hutuambia kuwa hapa tumekosea na hutuacha katika point ya kuhukumiwa na makosa
tuliyoyafanya. Kwa lugha nyingine maana yake, dhamiri zetu huzaa hatia mara
baada ya sisi kuingia katika kutenda kosa flani.
Mapungufu au athari ya dhamiri
Sio
tuu kwa dhamiri, kiujumla anguko la
mwanadamu, liliathiri sura nzima ya Mungu kwa mtu. Hivyo kuanzia utashi,
dhamiri na mengine yote ambayo yalikuwa yakiakisi sura ya Mungu kwa mtu
yaliathiriwa. Na ndio kuanzia point hii, mtu hakutakiwa kuitegemea akili wala
mawazo yake katika kumpendeza Mungu maana anguko/dhambi lilitia athari sura ya
Mungu kwa mtu.
MWANZO
8:21c “Maana mawazo ya moyo wa mwanadamu
ni mabaya tangu ujana wake;
Kwakuwa
tayari anguko/dhambi imezitia giza dhamiri zetu hii huweza kupelekea mtu kuwaza
kuwa jema ni baya na baya ni jema. Yohana 16:2-3, “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu
awuaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watayatenda kwasababu hawakumjua
Babab wala mimi”. Au kwa namna nyingine ningeweza kusema, watayatenda
kwasababu sura ya Mungu haipo tena ndani yao.
Hivyo,
mara baada ya anguko la mwanadamu katika bustani ya Edeni, mwanadamu anatakiwa
kutembea katika namna ambayo hatakiwi kabisa kuyaamini hata mawazo yake
mwenyewe maana yanaweza kumpeleka katika upotevu.
Hivyo
katika uumbaji wa pili ambao Mungu anaufanya katika Roho Mtakatifu, anakusudia
kutupa Roho Mtakatifu ili awe si tuu mbadala wa dhamiri zetu, lakini awe na
atende zaidi ya dhamiri zetu zilivyokuwa zikitenda. Ukikosa umakini, unaweza
kuhisi kazi ya dhamiri na Roho Mtakatifu ni sawa. Lakini katika somo hili nitakuonesha
utofauti mkubwa sana kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu
“Naye
akiisha kuja, hyo atauhakikishia ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na
hukumu”
YOHANA 16:8
Kama
dhamiri, Roho Mtakatifu yupo kutawala kiwango cha utakatifu wa mtu na kuhakikisha
mtu anakuwa mtakatifu kama Mungu alivyo mtakatifu.
Lakini,
zaidi ya dhamiri, yeye Roho Mtakatifu, ana uwanda mpana zaidi. Haiishii
kukuonesha lipi ni baya na lipi ni jema na kukuachia hukumu moyoni, bali yeye
hupiga hatua nyingine ya zaidi ya kukwambia namna unavyotakiwa kutenda ili
kutoka chini ya hiyo hukumu, na zaidi kabisa hukuombea ili utoke chini ya hiyo
hukumu.
“Kadhalika
Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, maana hatujui kumba itupasavyo; lakini Roho
mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”
WARUMI 8:26
Yohana
16:8 tulioiona hapo juu, inatueleza kuwa Roho Mtakatifu huuhakikishia ulimwengu
kwa habari ya dhambi (kwa neno la kingereza, convict au prove), jambo
linaloweza kumaanisha:-
·
Hufunua hatia ya ulimwengu/huutia ulimwengu hatiani
·
Humleta mtu katika point ambayo atakubali kuwa yeye ni
mkosefu
·
Hutumia ushahidi kamili, kumtia mtu hatiani
Lakini,
kinacho nifurahisha zaidi ni kwamba hufunua thamani ya mtu kwa Mungu, hata
katika mazingira ambayo yanamfanya asione thamani yake na kukosa ujasiri wa
kumsogelea Mungu kama Baba. Hivyo, Roho Mtakatifu, huwa mshauri wa kumuongoza
mtu katika mashauri yote ya ki-Mungu.
NAMNA DHAMIRI NA ROHO MTAKATIFU
VINAVYO SHUGHULIKA NA HATIA
AINA KUU MBILI ZA HATIA
1.
Hatia ya uongo
Kitabu
cha Mathayo 27:1-10 kinaeleza kuhusu habari ya Yuda Iskariote na mwisho wa
maisha yake. Yapo mambo kadhaa hapa natamani tuyaone:-
·
Ni kweli Yuda alitenda dhambi iliyozaa hatia ambayo ilimtesa
hata mara baada ya siku aliyoitenda ile dhambi kupita
·
Hatia yake, aibu na hukumu ilielekezwa kwake mwenyewe na
kumfanya aanze kujichukia, kujiona duni na kujiona hakuna aina ya msamaha
anayoweza kuistahili
·
Hili lilipelekea ajiue
Ninapozugumza
kuwa hatia hii inaitwa hatia ya uongo, wala
simaanishi kabisa kuwa mhusika hakutenda dhambi husika na hatakiwi kuwajibishwa
katika dhambi yake. Ninacho maanisha hapa ni kwamba, ni hatia ya uongo kwa
sababu kuwajibishwa huku kunatokana na chanzo kisicho sahihi kufanya hivyo
ambacho ni Dhamiri.
Nathubutu
kusema, si chanzo sahihi, kwasababu badala ya kukuinua katika kuanguka kwako,
kinazalisha chuki, hukumu na hasira juu yako mwenyewe kama ilivyotokea kwa Yuda
Katika
Galatia 2:8-14, Paul anatuambia kuwa ilimpasa kumkemea Kefa (Petro kwa jina
lingine), ambaye alikuwa anajua wazi kuwa msingi wa wokovu au neema ya Kristo
haupo katika utaifa, lakini upo katika Imani. Paul anasema Petro alikuwa
mnafiki, kwasababu alipokuwa akikutana na watu wa mataifa (wasio wa Israeli),
aliweza kuchangamana nao vizuri na kufanya shughuli kadhaa wa kadha wakiwa
pamoja, lakini aliposikia tuu watu wa Yakobo (Waisraeli) wanakuja, alijihukumu
na kuacha kuchangamana nao, jambo ambalo Paul analiita ni unafiki.
Lakini
hii ni kwasababu, Petro aliruhusu dhamiri/mawazo yake yaamue nini anatakiwa
afanye. Kila mara tunapoziacha dhamiri zetu zishughulike na makosa yetu, lazima
tujue kuwa huwa tunakuwa katika hali mbaya sana.
Ukweli
kuhusu hatia ya Uongo
I.
Huzalishwa ndani yetu kupitia dhamiri zetu na shetani
huishikia bango ili tusipige hatua mpya
II.
Ni hatia ya uongo kwasababu hukudanganya juu ya Mungu alivyo.
Wengi wanaopitia katika hali hii ya kushtakiwa, wamefika hatua hata ya kumuona
Mungu kuwa hana upendo, hataweza kusamehe na amechoshwa na madhaifu ya mtu kitu
ambacho ni uongo mtupu.
III.
Huifanya aibu, kudharauliwa, kuhukumiwa na kila baya, lielekezwe
kwa mhusika na kumfanya mhusika aanze kujichukia yeye badala ya kuichukia
dhambi.
“Kama
mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi”
ZABURI 103:12
“Atarejea na
kutuhurumia, atayakanyaga maovu yetu, nao utazitupa dhambi zao zote katika
vilindi vya bahari”
MIKA 7:19
“Kwasababu
nitawasamehe maovu yao, na dhambi zao sitazikumbuka tena”
EBRANIA 8:12
“Hata
imekuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita,
tazama yamekuwa mapya”
2WAKORINTHO 5:17
Maandiko
haya yote, yanaelezea ni kwa namna gani Mungu huitazama dhambi ambayo imekwisha
kutubiwa tayari. Tendo la kuishi na hatia ya dhambi uliyoitenda miaka kadhaa
iliyopita, ni maamuzi yako binafsi.
2.
Hatia ya Kweli
Hii
ni hatia ya kweli kwasababu huzalishwa na chanzo sahihi ambacho ni Roho
Mtakatifu, na ye eye hata mara baada ya kushuhudia kuwa u mkosaji, huwa
hakuachi katika point hiyo hiyo uendelee kujihukumu. Yeye hukuinua na
kukupeleka moja kwa moja kwa Mungu kama Baba yako na sio kama jemedari wa jeshi
au hakimu.
Ukweli
kuhusu hatia ya Kweli
I.
Huzalishwa ndani yetu na Roho Mtakatifu, jambo linalo
mkosesha shetani nafasi ya kuitumia kinyume nasi
II.
Aibu, hukumu, kudharauliwa, na kila baya litokanalo nayo,
huelekezwa kwa dhambi husika na kumfanya mtu aichukie dhambi na sio kujichukia
yeye mwenyewe.
III.
Kupitia hii, Roho Mtakatifu humuinua mtu huyu na kumfanya
aione thamani yake na aone hakuna kosa lolote lililokubwa kuzidi wingi wa
rehema, neema na upendo wa Mungu kwa mtu.
IV.
Kupitia hii, Roho Mtakatifu hutuonesha kuwa tu wapekwe na
hatuwezi kuendele maana tumetengwa na Baba na hutuonesha namna ya kumrudia
V.
Kupitia hii, Roho Mtakatifu hutuongoza katika kweli yote
NIFANYE NINI NINAPOSHAMBULIWA NA
HATIA YA UONGO
1.
Lazima uelewe kuwa, unashambuliwa na hatia ya uongo kwasababu
ni kweli kuna mahali umekosea au ulikosea. Shetani ni mshtaki wetu, lakini
hawezi akakushtaki kama hakuna mahali ulipolegeza viwango vya utakatifu na
kumkosea Mungu.
2.
Wapo baadhi ya walimu na wachungaji wangekupa hatua ya
kuingia katika maombi, lakini mimi naomba nikupe hatua muhimu sana kabla ya
hiyo kuwa JIPENDE. Usiruhusu kamwe chuki
na kujiona duni ambako hatia ya uongo inakuletea kuwe ni sehemu ya maisha yako.
Hata kama ni kweli umekosea na unarudia kosa hilo mara nyingi, siri ya kwanza
ni kujipenda. Kadri unavyojipenda, utaitambua thamani yako, na hautaruhusu
kamwe dhambi ishushe thamani yako. Ukijipenda, utaweza pia kujiombea.
3.
Fanya mipango na maamuzi ya kuamua kuiacha dhambi unayoifanya
na kutengwa na hatia inayozaliwa. Hatua na mipango hii, ndiyo hasa huhitaji
maombi ya kujitamkia kutengwa na hatia yako. Mruhusu Roho Mtakatifu akuongoze
katika njia na namna atakayo wewe na sio vile mawazo vako yanakutuma
“Basi mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kwelikweli”
YOHANA 8:36
NATAMKA UHURU JUU YAKO KATIKA JINA LA
YESU KRISTO
©Pastor Sam Gripper –
TAG PENUEL ASSISTANT PASTOR
TOTAL TRANSFORMATION ©2018
0657670972
©Pastor Sam Gripper –
TAG PENUEL ASSISTANT PASTOR
TOTAL TRANSFORMATION ©2018
0657670972
No comments:
Post a Comment