THE WAIT – KUSUBIRI
January 14, 2018
UTANGULIZI
Kwa
kawaida kabisa, hapana mtu ambaye anapenda kusubiri. Kila mtu hutamani kila
anachokifanya au anachopanga kukifanya kifanyike ndani ya majira na wakati
aliopanga tena kwa haraka.
Ukienda
bombani kuchota maji, hautatamani ukute foleni, utatamani uchote na kuondoka,
ukienda bank kufanya aina yoyote ya malipo, hutafurahia kukuta foleni ambayo
itakufanya usubiri, ukienda kituo cha basi na basi lisipowasili katika muda
uliotarajia, utajisikia vibaya na kukasirika kwakuwa unatakiwa kusubiri,
unapopiga simu kwa rafiki yako, na ukakuta anaongea na simu nyingine na unatakiwa
kusubiri lazima utakasirika tuu, unapopiga simu ya huduma kwa wateja na ukakuta
mhudumu hapokei kwasababu anaongea na simu nyingine na unatakiwa kusubiri, ni
wazi tuu utakasirika.
Hii
yote ni kwasababu kusubiri ni jambo gumu sana lenye gharama ambalo mara
nyingine hupima na kujaribu kiwango cha kuamini cha mtu. Na kiwango cha kuamini
kinapopimwa au kujaribiwa, maana yake kiwango cha uwezekano wa kuwezekana au
kutowezekana kwa mambo yanayotarajiwa au kusubiriwa kinapimwa na kujaribiwa
pia.
“Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia
kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya!
Katufanyizie miungu itakayo kwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa
katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata.”
KUTOKA 32:1
MUNGU HUTAKA
TUSUBIRI KWA SABABU:
·
Ipo Ahadi
Kimsingi,
hapana kusubiri kama hapana ahadi inayotakiwa kusubiriwa. Mungu yupo na ahadi
nyingi sana kwaajili yetu ambazo zimefunuliwa kupitia Neno lake. Kwa kukaa
chini ya Neno lake, tunafanywa wangojezi kwa namna ya subira inayoleta tumaini
na wamiliki wa ahadi hizo kabla hazijadhihirika, kwa njia ya imani. Hivyo,
Mungu anataka tusubiri kwakuwa Ipo ahadi.
·
Yeye ndiye
aliyeahidi
Kujua
kuwa ipo ahadi, ni jambo la msingi na la thamani sana kwakuwa linatupa tumaini.
Lakini kujua kuwa Mungu ndiye aliyeahidi hizo ahadi, ni jambo ambalo linatupa
ujasiri wa kusimama thabiti katika kusubiri kwetu hata kama tutapita katika
nyakati ngumu mno, kwasababu tuu ahadi zetu zimetoka katika chanzo chenye tabia
ya uaminifu, ukweli na kutobadilika.
Hivyo katika point hii, Mungu anatuinua kutoka katika kiwango cha kuitazama na
kuisubiri ahadi hadi kiwango cha kumtazama na kumuangalia aliyeahidi na tabia
zake.
“Nitakusujudu
nikilikabili hekalu lako takatifu, Nitalishukuru jina lako, kwa ajili ya
fadhili zako na uaminifu wako, kwa maana umeikuza ahadi yako, kuliko jina lako
lote”
ZABURI 138:2
·
Ana nia na
mpango thabiti juu ya kila anacho ahidi
Mara
nyingi huwa napenda kuzungumza na rafiki zangu, kuwa Mungu hafanyi chochote
anachokifanya kwasababu tuu ni Mungu, ni mamlaka iliyo kuu na hapana mamlaka
yoyote ya kuuliza utendaji wake, bali nguvu inayomsukuma afanye chochote anachotaka
kukifanya ni nguvu ya Kusudi.
Hapana
jambo anafanya pasipo kuwa na kusudi. Mwanzo 1:26, anaeleza wazi juu ya mpango
wake wa kumuumba mtu. Anasema atamuumba kwa sura na kwa mfano wake, tofauti
kabisa na alivyo viumba viumbe vingine vyote. Na hii haituambii tuu juu ya aina
ya mtu ambaye Mungu anakusudia kumfanya, lakini zaidi mpango juu ya aina ya
maisha ambayo Mungu amekusudia mtu huyu aje kuyaishi.
Hivyo
Mungu anaujua mpango wa ahadi yako vizuri kuliko wewe ujuavyo na yupo committed
kuitimiza, pengine kuliko ambavyo wewe upo committed kuipokea, na pia alikuumba
kutokana na ahadi aliyonayo juu yako. Kwa lugha nyingine, kabla ya wewe kuwepo
ilikuwepo kwanza ahadi au kusudi, ambalo lilihitaji Mungu akuumbe hivyo ulivyo
ili kufit katika kusudi/ahadi
·
Anafanya
kazi zake katika majira na nyakati zake yeye mwenyewe.
Hii
ni sababu nyingine ya muhimu ya kwanini Mungu anataka tuwe na tabia ya
kumsubiri. Mwanzo 1:1, inaposema “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi,
haimaanishi kuwa huu ndio ulikuwa mwanzo wake, lakini alikuwepo kabla ya wakati
na anachokifanya hapa ni kuuanzisha wakati na kutuweka sisi chini/ndani ya
wakati na majira husika.
Hivyo
yeye anatuongoza katika nyakati zetu kwa kutawala mambo yaliyo nje ya nyakati
zetu. Hivyo, tunatakiwa kumsubiri maana mambo tunayoyatarajia yapo nje ya
nyakati zetu lakini ndani ya nyakati zake.
“Akawaambia,
Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake
mwenyewe”
MDO 1:7
Sababu
hizi za Mungu kutaka tutengeneze tabia ya kusubiri ni sababu ambazo kimsingi zinatuchukua na
kutuweka mahali ambapo tunajikuta ili kupokea ahadi zake, ni lazima tumtegemee
kwa asilimia zote ili atende. Lakini mara nyingi tumekuwa na udhaifu wa kuziona
sababu hizi zote kwamba zinatusaidia kumtegemea Mungu, badala yake tumekuwa na
mitazamo ya tofauti juu ya sababu hizi.
MWANADAMU
(KINYUME NA MUNGU) HUTAKA KUSUBIRI KWA SABABU:
·
Anajua ipo
ahadi
·
Yupo na
motives au nia binafsi juu ya ahadi tarajiwa
·
Ana wakati
binafsi ambao anataka ahadi itimie
Katika
mambo haya matatu hakuna mahali ambapo mwanadamu huweza au hutamani kuuona
uaminifu wa Mungu kwa ukubwa kuliko ahadi tarajiwa. Ni katika point hii ambapo
mwanadamu hushindwa kusema “Ahadi yangu itimie au isitimie kwa wakati
niliotaka, bado Mungu ni mwaminifu, ahadi zake ni amini na kweli, na nitasubiri
chini ya wakati wake ayadhihirishe mapenzi yake”
Na
hii ni kwasababu anatarajia ahadi ya Mungu lakini anataka idhihirike kwa
mapenzi yake binafsi na wakati wake ambao yeye (mwanadamu) anataka na sio
Mungu. Na ndio maana sababu 4 za Mungu kutaka tuwe na tabia ya kusubiri ni
tofauti na sababu zetu za kusubiri.
“Hata
mwaomba, wala hampati kwasababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tama zenu”
YAKOBO 4:3
Nilipata
kibali wakati Fulani, kutembelea mahali Fulani kwaajili ya kufanya huduma na
nikabahatika kusikia shuhuda za nini Mungu aliwatendea watu wakati kipindi cha
ushuhuda kinafanyika baada ya mimi kuhudumu.
Akasimama
binti mmoja ambaye alitoa ushuhuda kuhusu uhitaji wa kaka yake kupata ajira, na
vile ambavyo huyu binti alikuwa akifunga na kuomba mara kwa mara ili kumwomba
Mungu kwaajili ya kaka yake. Katika maelezo yake huyu binti akasema, ilifika
point ambayo yeye alichoka kuendelea kuomba na akamuwekea Mungu kile
alichokiita yeye “deadline” kuwa hadi siku flani Mungu asipojibu, yeye
hataombea hilo jambo tena.
Nilishtuka,
kwasababu kwangu mimi kilikuwa ni kitu kigeni sana. Nikakumbuka wakati ambao
Yesu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake kuomba, aliwapa maneno ya msingi sana
“Utakalo lifanyike hapa duniani, lifanyike kama lifanyikavyo mbinguni”.
Nikagundua kuwa huyu binti, alionesha tabia ambazo wanadamu wote huonesha.
Kutafuta ahadi za Mungu huku tukimfunga atende katika nyakati zetu na kwa
ukubwa ambao sisi tunauona.
Hivyo
hata katika hali yetu hiyo ya ujinga Mungu anapotenda kwa sababu yeye yu
mwaminifu, naweza kusema hutenda kama vile sisi tunavyotaka na sio vile yeye
alivyokusudia. Hivyo kuziweka nyakati zetu na motives zetu katika ahadi za
Mungu, ni sawa na kumzuia Mungu afanye kwa ukubwa aliokusudia yeye.
Wakati wowote, kiwango
unachotakiwa kusubiri, kinapozidiwa na shauku yako binafsi ya kutaka ahadi
idhihirike hata kabla wakati wa Mungu haujafika, Unashambuliwa na Tamaa
|
MWANZO
16:1-6, Inaeleza kuhusiana na kushindwa kusubiri kwa Sarai mkewe na Abram
kunakofanya Sarai amruhusu Abram kuzaa na kijakazi, jambo ambalo linakuja kuwa
mwiba kwa maisha ya Sarai na Abramu kabla ya mtoto kuzaliwa na hata mara baada
ya mtoto kuzaliwa (Ishmael) na Yule mtoto wa ahadi (Isaka) anapokuja kuzaliwa.
Na
sehemu kubwa ya uadui ambao upo hata hivi leo kati ya Waarabu na Waisrael, ni
matokeo ya mtoto asiyekuwa wa ahadi (Ishmaeli) kuzaliwa kabla ya mtoto wa ahadi (Isaka), kwasababu tuu
wazazi walishindwa kusubiri.
“Kwa maana
imeandikwa ya kuwa Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja
kwa mwungwana. Lakini Yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, Yule wa mwungwana
kwa ahadi”
GALATIA
4:22-23
MAMBO MAWILI
YANAYOFANYA KUSUBIRI KUONEKANE NI KUREFU NA KUGUMU
1.
Uncertainty
(kutokuwa na uhakika)
2.
Hofu ya
kupoteza ahadi
Hebu
fikiria, rafiki yako wa muda mrefu anapokupigia simu na kukwambia anakuletea
zawadi ambayo hataki kuitaja ni nini. Katika hali hii, itakuwa ni ngumu sana
kwako kumsubiri kwakuwa unashauku ya kutaka kujua anakuletea nini, na hata
akikwambia umfuate popote alipo utakubali kwakuwa tuu, hujui amekuletea nini na
ungetamani kujua. Hivyo utaona tuu ni kama muda hauendi hivi.
Jambo
la ajabu ni hili, utakuwa na shauku sana ya kutaka kujua amekuletea nini
kwasababu huna uhakika lakini utakuwa na hofu ya kuipoteza ahadi ya kitu usichokijua/usichokuwa na uhakika
nacho.
Hivyo
kikawaida, kusubiri kwetu huonekana ni kwa muda refu sana kwasababu tuu hatujui
tunasubiri nini, lakini huwa tunahofu ya kupoteza ahadi tunayoisubiri ambayo
kimsingi hatujaijua bado. Kimsingi, mambo tunayoyasumbukia katika maisha yetu
ambayo ndiyo hasa hutufanya tuone kusubiri ni jambo gumu sana na linahitaji muda
mrefu mno ni mambo ambayo sio msingi wa maisha yetu lakini huwa tunahofu ya
kuyapoteza.
Mstari 25d “Maisha
je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?”
MATHAYO
6:25-34
“Msijisumbue
kwa neno lolote; bali katika kila neon kwa kusali na kuomba pamoja na
kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu ipitayo akili
zote itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu - WAFILIPI
4:6-7
“Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe, katika njia
zako zote mkiri yeye, naye atanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni
pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu -MITHALI 3:5-7
MAMBO 6
MUHIMU AMBAYO KUSUBIRI HUFANYA KATIKA MAISHA YETU
1.
Kusubiri
hufunua nia zetu za ukweli.
Watu ambao hawana nia njema, iwe ni kwenye
kazi, mahusiano nk. Hawawezi kusubiri muda mrefu kwasababu hawafurahishwi kuwa
committed kusubiri jambo litokee, lakini hufurahishwa na hutamani kuona matokeo
ya haraka
Mwanzo 11:1-6, inaeleza vema. Wale wajenga
mnara walipokuwa na nia ya kwenda kinyume na ahadi ya Mungu kuwatawanya juu ya
dunia nzima, waliona hapana haja ya kuisubiri hiyo ahadi hivyo wakajenga mnara
ili wasitawanywe, wajifanyie kumbukumbu lao. Lakini walipoanza kujenga ni kana
kwamba walikuwa na nia nzuri ya kufika juu kabisa mbinguni lakini wakati,
ulielezea nia yao.
Watu wenye nia njema, husubiri.
2.
Huzaa moyo
wa shukrani
Kitabu cha Yohana 9:1-41, utaona ni kwa kiasi
gani huyu kipofu tangu kuzaliwa alivyokuwa na furaha na kiwango kikubwa cha
shukrani, mara baada ya Yesu kumponya. Muda aliotumia katika kuamini na
kuisubiria ahadi, ulibeba ukubwa wa shukrani yake.
Wengi hatuna mioyo ya shukrani kwasababu zile
nyakati ambazo ilitakiwa tumsubiri Mungu afanye, sisi tulirush na kufanya
wenyewe, tunapojipatia kina Ishamel kama Abram, hatuwezi kuwa na moyo wa
kushukuru maana si mwana wa ahadi iliyo tarajiwa.
Hivyo, kusubiri, huzaa moyo wa shukrani kwa
yale ambayo Mungu ametimiza
3.
Huimarisha Imani
“Wapenzi,
sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini, twajua
ya kuwa, atakapo dhihirishwa tutafanana naye; kwa maana tutamuona kama alivyo.
Na kila mwenye matumaini haya katika yeye, hujitakasa kama yeye alivyo
mtakatifu.
1YOHANA
3:2-3
Huu
ndio hasa msingi wa Imani yetu. Hatutakiwi kuchoka kusubiri, maana mbali na
ahadi za kubarikiwa na kuwa vichwa tunazozingojea, ipo ahadi kuu zaidi ambayo
ndiyo msingi wa Imani yetu, kudhihirishwa kwa Mwana wa Mungu ili tumfanane.
Lakini, katika kusubiri ahadi hii, lazima tukubali kuuishi kana kwamba imekuwa,
tuishi kwa utakatifu kama yeye alivyo.
4.
Hubadili
tabia zetu
“Ilikuwa
hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa
njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; Maana Mungu alisema,
Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapo kutana na vita, na kurudi Misri.”
KUTOKA 13:17
Ilitakiwa
Israeli wazungushwe na kusubiri sana jangwani, kwa muda wa miaka 40 ili Mungu
abadili tabia zao. Kama asingewafanya wasubiri, akawaruhusu wapiti kwa njia
fupi, wangekutana na vita, wasingekuwa mahodari na majasiri kupambana hadi
mwish. Lakini Mungu aliwazungusha ili kutoa roho ya woga, na athari ya utumwa
ndani yao ili wawe mahodari.
5.
Huimarisha
ushirika na Mungu
Baadhi
ya mahusiano imara na ya kweli tuliyo nayo, ni kwasababu ya mmoja wa rafiki
kuweza kusimama imara na kwa ukaribu sana, katika nyakati ngumu ambazo tuliwahi
kupitia.
Tunajifunza
kuhusiana na watu wakuu katika maandiko ambao walitakiwa kusubiri ahadi za
Bwana kutimia kwao kwasababu suala zima la kusubiri ahadi halikuwa ni mpango wa
haraka haraka wa kusubiri siku kadhaa na kupata waliyosubiri lakini lakini
walihitaji kwanza kukaa katika ushirika na Mungu kwa namna kubwa sana hata kama
ingegharimu maisha yao yote.
Daudi,
kwa mfano, alitawazwa kuwa mfalme wa Israel akiwa na umri mdogo tuu, lakini
ilitakiwa asubiri tena akiwa katika mahusiano imara na Mungu, miaka mingi sana
mbele ili kukalia kiti cha ufalme. Yusufu pia, alikuwa na ndoto lakini
ilimgharimu mambo mengi sana hadi ndoto kutimia, na kwa wakati wote wa kusubiri
ndoto itimie, alitakiwa kuishi maisha yanayo akisi uimara wa ushirika wake na
Mungu
Hivyo
katika kusubiri, si mbaya sana kama utaitazama sana ahadi, lakini ni nzuri
zaidi kama utamtazama mtoa ahadi na kujenga ushirika nae.
6.
Hutengeneza
uvumulivu
Mungu
anapoiangalia ahadi aliyokuahidi, haioni kuwa ni kubwa na muhimu sana kama
kukusubirisha ili akutengenezee misuli ya uvumilivu. Na hili, lifanye hata
shuhuda zetu zibadilike. Tunapokuwa tumemwamini Mungu katika ahadi flani kubwa,
na ikatokea hajafanya kwa wakati tulio tegemea, tusikatishwe tama. Tumshukuru
maana ametutengenezea misuli ya uvumilivu jambo ambalo ni kubwa kuliko ahadi
iliyo ahidiwa.
Ibrahimu,
alikaa muda mrefu sana kumngojea Isaka. Na alipokuja Isaka, Ibrahim alikuwa
tayari na misuli mikubwa sana iliyotokana na kusubiri, kiasi ambacho hata
alipoambiwa akubali kwa makusudi kuipoteza tena ahadi aliyoingoja miaka mingi
(kumtoa Isaka sadaka), hakusita.
TAG PENUEL LUHANGA – JABA
©Sam Gripper 2018, Assistant Pastor
0657 670972
No comments:
Post a Comment