MAOMBI NA UTII


MAOMBI NA UTII

Pastor Sam Gripper

28th January 2018

UTANGULIZI

Nilikuwa katika kutafakari na ikanibidi nifike point ambayo natakiwa kukubali kuwa moja kati ya mambo magumu sana ambayo wanafunzi wa Yesu walimwomba Yesu awafundishe kuyafanya ni namna ya kuomba. Sijui nguvu gani nyuma iliyo wasukuma katika kufanya hilo, lakini naweza kuhisi kuwa walihitaji kufundishwa namna wanavyoweza kujipatia mahitaji yao kutoka kwa Mungu kama wanavyohitaji.

Lakini jambo gumu sana ni jambo ambalo Yesu anawafundisha kuwa wanatakiwa kuomba na kutegemea mahitaji yao kwa Mungu, sio kama wao wanavyohitaji lakini kama Mungu apendavyo kuwapa. MATHAYO 6:10 “Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama mbinguni”.

Hakuna mahali pagumu sana na panapohitaji Imani ya kweli na uthabiti wa mahusiano kati ya mtu na Mungu, kama mahali ambapo upo kwenye uhitaji, unajua ni nini unakihitaji kwa huo uhitaji ulio nao, lakini unatakiwa umwache Mungu ambaye kikawaida kabisa hayupo katika hali unayopitia, afanye sio kama wewe unavyotaka, lakini kama yeye anavyotaka. Wasiwasi mkubwa unaozaliwa hapa ni, “Je, anajua exactly nini nahitaji kwa hali hii na atafanya kama vile ninavyohitaji?”

Katika point hii, pana mtego sana. Ndipo Yakobo 4:3 inasema “Hata mwaomba, wala hampati, kwa sabababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.





“Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke, walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe”

MATHAYO 26:39

Narudia kuandika tena, katika point hii panahitaji uthabiti na uimara wa mahusiano binafsi kati ya mtu na Mungu kiasi ambacho mtu ataamini kuwa mapenzi ya Mungu hata kama hayatakuwa sawa na uhitaji, bado ni sahihi na kamili kwa kusudi alilonalo Mungu kwa mtu.

Hitaji kuu la Yesu katika maandiko hayo, ni kutoka katika adhabu inayomkabili. Lakini, mapenzi ya Mungu kuhusiana na hali hiyo husika ni tofauti kabisa,  na kwasababu Yesu amekwisha omba kuwa Mungu atende kama anavyotaka, hana budi kukubali na kupokea nini Mungu anataka kifanyike kwa hali iliyo mbele yake.

Ni mara chache sana (wala simaanishi haiwezekani), Mungu huwa anaweza kuruhusu maombi yetu yabadilishe nia na mtazamo wake juu ya jambo flani. Na hufanya hivyo kwa makusudi maalum na wakati maalum. Lakini mara zote, Mungu huhitaji maombi yetu yawe katika msingi wa kufunua na kutafuta mapenzi yake kwetu na kwa hali tunazopitia na sio kumshawishi atende nini sisi tunataka.

 Tatizo la mwanadamu, ni kutokuamini kuwa mapenzi ya Mungu yanaweza kukidhi uhitaji alionao. Na sio kwamba hamuamini Mungu, lakini ni kwamba haamini kuwa katika hali ya uhitaji anayopitia, Mungu pia anapita na yeye katika hali hiyo na lolote atakalo litenda ni jema sana.

“Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani ya kwamba, hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani. Na Baba yenu wa mbinguni, huwalisha hao. Ninyi je!, si bora kupita hao?”

MATHAYO 6:25-26



Maandiko haya hayamaanishi kuwa Mungu hataki tujishughulishe na wajibu wetu wa kila siku katika maisha. Anataka sana, asichokitaka ni katika hatua ya kutimiza wajibu wetu wowote, tuzitegemee akili zetu. Alipo mwambia Adam na Eva kuwa wasile matunda ya mti wa maarifa, sio kwamba hakutaka wawe na maarifa, lakini alitaka kwa utayari wao kutii, yeye (Mungu) awe chanzo cha maarifa kwao na mwanadamu amtegemee yeye kwa maarifa ambayo hayakuwa na uovu ndani yake.

Kuwa tayari mapenzi ya Mungu yatimizwe kama yeye atakavyo, kuna gharama. Na moja kati ya gharama hizo ni utayari wa kutii nini Mungu kupitia mapenzi yake anataka kifanyike.



MAANA YA UTII

Kwangu mimi, utii ni zaidi ya kufanya ulichoagizwa kufanya au kuacha ulichokatazwa kufanya. Utii unachukua maana zaidi ya hapo, na katika chapisho hili, nitautafsiri utii kama mlango wa Mungu kudhihirisha mapenzi yake kwa mtu aliyemwomba.

Tunapomuomba Mungu, tunaomba mapenzi yake yadhihirishwe, lakini namna pekee ya Mungu kudhihirisha mapenzi yake, ni sisi kuchukua hatua ya kuishi sawa na kutenda sawa na anavyotaka. Katika maandiko hapo juu, tumeona Yesu akiomba kikombe cha adhabu kimuepuke (hivi ni jinsi yeye alivyotaka), lakini aliacha Mungu adhihirishe mapenzi yake katika hilo na hata mara baada ya Mungu kudhihirisha mapenzi yake, alikuwa tayari kuyatii.

Watu wengi hupenda kuomba (jambo ambalo kimsingi sio baya), lakini sio wote huwa tayari kufuata maelekezo ambayo Mungu huwapa kama namna ya kupokea majibu yao. Hivyo utii, ni jambo pekee ambalo litamruhusu Mungu kudhihirisha mapenzi yake kwa utayari wa mhusika kukubali na kutenda nini ataamriwa atende.





MAMBO MAKUBWA MAWILI YANAYOPIMA KIWANGO CHA UTII CHA MTU

Jambo la kwanza ni Mambo unayoyapenda au kuyafurahia kufanya, na pili ni mambo usiyoyapenda na hufurahii kuyafanya. Sio mara zote tunapomuomba Mungu, huwa anajibu katika namna tunayoipenda au kuifurahia au sio kila mara zote hutoa majibu tunayoyapenda. Waala simaanishi Mungu hajui nini tunahitaji na wala hawezi kufanya sawa na tunavyohitaji. Lakini mara nyingine, mapenzi yake huwa ni bora sana katika macho yake mwenyewe kuliko shauku zetu.

“Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”

AYUBU 2:10

Kiwango cha utii wa mtu, huanza kupimwa katika eneo kama hili.  Mahali ambapo uliyotarajia kuyapata kutoka kwa Mungu ambayo kimsingi unayapenda na kuyafuahia ni tofauti na yaliyokuja, na unatakiwa uyakubali na uyaishi pamoja na kwamba yamekuja katika namna ambayo hukuitarajia au huifurahii.

Utii wetu hauhesabiwi peke yake kwa kufanya mambo tunayoyapenda, lakini kama utakutana na mambo usiyoyapenda na ukatakiwa uyakubali kwasababu ni mapenzi ya Mungu kwako, utakuwa tayari kuyafanya?

Ukweli wa msingi sana kuhusu mambo tunayoyapenda au kuyafurahia, ni kwamba huturidhisha na kutufanya tujione tupo mahali flani ambapo tulitakiwa kuwa. Ukiwa na rafiki ambaye anakupenda na kukufurahia, sio mara zote ataweza kukwambia ukweli utakaokuuma, maana anajali kuhusu wewe na anaogopa kukuumiza. Hivyo kwa namna hiyo, utajiona ni mkamilifu na huna haja ya kutia bidii katika kuwa mtu bora zaidi maana hapana mtu anayezinyoshea vidole kasoro zako.



Ni lazima mara nyingine kwasababu tuu tumeomba mapenzi ya Mungu yadhihirike, tuwe tayari kutii na kuamini kuwa chochote alichokidhihirisha na kukileta kwetu kama majibu ya maombi yetu, ni chema sana. Si tuu tufurahi kupokea mambo tunayoyafurahia, lakini pia hata tusiyoyafurahia.

Tunafahamu kuwa Ibrahim alikuwa akimsubiri Isaka kama ahadi ya Mungu kwa muda mrefu sana. Na miaka michache mara baada ya Mungu kumpa majibu yake, Mungu akahitaji tena Ibrahim amtoe Isaka (mwana wa pekee). Hii ilikuwa ni namna ya Mungu kupima utii wa Ibrahim kwa kugusa kitu ambacho Ibrahim anakipenda na kukifurahia.

Hatutatii hadi tutakapo kubali kuyaacha mambo tunayoyafurahia na kuyapenda kwa shauku zetu, ili tutimize mapenzi ya Mungu na pale tutakapo takiwa kukubali kutii juu ya mambo tusiyopenda wala kuyafurahia kwaajili ya mapenzi ya Mugu.

UTII HUFUNUA :-

1.     Kibali

“Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, name nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi, maana nimejipatia mfalme katika wanawe.”

1SAM 16:1

Jambo pekee lililofanya Mungu ahamishe kibali kutoka kwa Sauli na kukipeleka kwa Daudi, ni tendo la Sauli kukosa utii. Mungu alipomtuma Sauli akawaangamize Waamaleki, alienda na kuangamiza vitu na watu ambao hakuwapenda wala kuwafurahia machoni pake lakini Mfalme Agagi na mifugo mingine ambayo ilipata kibali machoni pake aliiacha hai. Utii wetu unapimwa kwa kukubali kuviharibu hata vitu tunavyovipenda kwaajili ya mapenzi ya Bwana.



Kwa kukosa kutii, Roho ya Bwana ilimwacha Sauli, na ninataka kuamini kuwa kwa tendo hili, hakuna maombi ya Sauli ambayo yangepata kibali maalum sana mbele za Mungu kama yalivyokuwa mengine yakipata kibali kabla hajamkosea Mungu. Hivyo kwa kutii Neno la Mungu, tunapata kibali cha kukubalika machoni pa watu, lakini zaidi machoni pa Bwana. Nimeandika lakini zaidi machoni pa Bwana, maana kuna nyakati kutii kwako mapenzi ya Mungu kunaweza kukukoseshe kibali machoni pa watu lakini kwa Bwana kitabaki vilevile.



2.     MAMLAKA

“Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi”

ISAYA 1:19

Siri ya mamlaka na nguvu ya utawala, imefungwa katika tendo la utii. Unapokosa kuyatii mapenzi ya Mungu na kufanya kinyume akuagizavyo, unapoteza nguvu ya mamlaka na utawala na kumpa shetani nguvu hii juu yako. Katika hali ya namna hiyo, hapana maombi utaomba maana u mtumwa, mtu asiyejua thamani na nguvu yake katika ufalme wa Mungu.

Mathayo 4:1-11, Yesu kama Adam wa pili, hakuweza kuipoteza mamlaka yake kiurahisi tofauti na Adam wa kwanza alivyotenda, kwasababu alisimama katika utii wa nini mapenzi ya Mungu yanataka afanye. Na kwa namna hiyo, aliweza kuitunza mamlaka na kwa sababu ya utii huu inakuwa ni rahisi na sisi kuipokea hii mamlaka kwasababu hakukubali kuipoteza kwa kukosa kutii nini Neno la Mungu lilikuwa likimuagiza.

Kati ya vitu vyote tunavyotakiwa kuviangalia kwa umakiini sana ili maombi yetu yajibiwe kikamilifu, ni suala zima la kutii.



© Pastor Sam Gripper 2018

#Betransfomed
Unknown
Unknown

This is a short biography of the post author. Maecenas nec odio et ante tincidunt tempus donec vitae sapien ut libero venenatis faucibus nullam quis ante maecenas nec odio et ante tincidunt tempus donec.

No comments:

Post a Comment