MLANGO
By Pastor Sam Gripper
4th March
2018
“10 Wala msinung’unike kama wengine wao walivyonung’unika wakaharibiwa na
mharibu. 11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili
kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. 12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama aangalie asianguke. 13 Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa
lililokawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe
kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa
kutokea ili mweze kustahimili
1KORINTHO 10:10-13
Imenipasa
kunukuu kuanzia mstari wa 10 ingawa mstari lengwa zaidi ni ule wa 13 ambao
unazungumza mambo makuu manne nitakayo yazungumzia katika somo hili. Mambo hayo
ni jaribu lililo kawaida ya wanadamu,
uaminifu wa Mungu, mlango wa kutokea na kustahimili.
Tukianzia
sura ya 10 na mstari wa 1 kabisa, tunaanza kuona Paul akifunua fundisho lililokuwa
chini au nyuma ya tendo la wana wa Israel kutolewa Misri, kupitishwa katika
bahari ya Sham na kuongozwa jangwani.
Tendo lao la
kuongozwa na wingu na kupitishwa katikati ya bahari Paul analizungumzia kuwa ni
fundisho juu ya ubatizo, kwamba Taifa lilibatizwa ili kuwa mali ya Musa,
Mwamba/nguzo ambayo ilionekana ikiwaongoza mara zote, na mara yingine hata
kutoa maji kwaajili yao, Paul anaufunua kama ni Kristo. Lakini mstari wa 6 Paul
anazungumza kuwa mambo haya yote yalitokea kwa namna ya mfano (kivuli ili
kuakisi maisha ya Kristo na kanisa). Mstari wa 11 pia Paul anarudia kusema kuwa
haya mambo yalikuwa ni kivuli na yakaandikwa ili sisi kama kanisa tujifunze na
tuonywe kwa hayo.
Kila mmoja
anapoingia katika shida, au jaribu la aina yoyote jambo la kwanza kabisa ambalo
anatamani litokee, ni mlango wa kutoka katika jaribu hilo. Na hapa,
ninapozungumza kuhusiana na jaribu, nazungumzia yale ambayo Mungu huwa anatupa
kuzipima na kuziinua Imani zetu nay ale ambayo yanatokana na tama zetu na
shetani anayatumia kututoa katika mstari ambao Mungu amekusudia tuwe.
“Mtu ajaribiwapo
asiseme ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu; wala
yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tama yake
mwenyewe, huku akivutwa na kudanganywa”
YAKOBO 1:13-14
[Kwa kibali cha Mngu nitakuja siku
moja kuandika juu ya utofauti wa majaribu (trials) yanayoletwa na Mungu na
majaribu (temptation) yanayotumiwa na shetani kutokana na tama zetu]
Lakini
katika aina yoyote ya jaribu alilonalo mtu, huwa jambo la kwanza ambalo
analihitaji, ni mlango wa kutoea.
Nitasimamia katika andiko letu la kwanza kutoka 1Korintho 10:13 kueleza mambo
kadhaa kuhusu mlango wa kutokea.
1.
Kila jaribu lina mlango wa kutokea
Inaweza
ikawa ni kauli nyepesi sana, lakini namwomba Mungu akufunulie maarifa ili
usiisome kwa wepesi. Jaribu, shida au tatizo huweza kuambatana na kuchukiwa,
kudharauliwa, kutengwa, kunyoshewa vidole, maumivu, kujidharau, kupingwa,
kuwekewa kila aina ya vizuizi, lakini pia huambatana na mlango wa kutokea.
Mungu
anapolileta au kuruhusu shida au jaribu kwako, hulileta na kuliruhusu kama
kifurushi kamili (a complete package). Na moja kati ya vitu vinavyofanya
kifurushi hicho kiwe kamili, mbali na shida na maumivu vinavyo ambatana na
tatizo hilo, ni uwepo wa mlango wa
kutokea. Kwa lugha nyingine ni kwamba kama ambavyo hakuna jaribu lisilozaa
maumivu, ndivyo ambavyo hakuna jaribu lisiloletwa na mlango wake.
2.
Kufunguliwa kwa mlango, ni jambo dogo
kuliko mafunzo uyapatayo kanla mlango haujafunguliwa
Kila mmoja
anayepita katika aina yoyote ya shida huwa na fikra ya kwamba jambo kubwa na
muhiu kuliko yote ni kufunguliwa mlango ili atoke katika shida hiyo.
Kufunguliwa mlango ni jambo dogo sana kuliko ukubwa wa maarifa unayotakiwa
kuyapata ndani ya gereza na kabla mlango haujafunguka.
Lengo la
Mungu kuruhusu upite katika eneo flani gumu, sio kukuacha tu na baadaye kukufungulia
mlango utoke kiurahisi. Yale atakayokuwa akikufundisha ndani ya gereza na kabla
mlango haujafunguka ndio hutafsiri wakati wa mlango wako kufunguka. Hivyo,
hakuna mlango kufunguka kama hakuna misuri iliyotengenezwa.
Katika
mstari 13, wa andiko letu kuu maandiko yanasema Mungu atafanya mlango wa
kutokea ili tuweze kustahimili. Maana yake kiwango cha ustahimilivu kitaamua
wakati wa mlango wako kufunguka na kitaamua aina maisha utakayoanza kuyaishi
ukiwa nje ya gereza.
3.
Sio kila mlango unaofunguka mbele
yako ni kwaajil yako
Inaweza kuwa
ni kauli tata na yenye kushtusha lakini nina uhakika juu ya hili. Tunaposoma
habari za Abramu katika kitabu cha Mwanzo 16:1-16, tunaona matokeo ya Sarai
kumlazimisha Abram kuingia katika mlango ulioonekana kana kwamba ni kwaajili
yake kupita na kumbe haukuwa wake.
Sara hakuwa
na uwezo wa kuzaa ingawa tayari Mungu alimuahidi Ibrahim kujitwalia uzao. Sara
pasipo nia mbaya, akauona mlango mwingine kwaajili yao kupata uzao ambao
ulikuwa ni Abram kumwingilia kimwili mjakazi. Ni jambo ambalo halikuufunga
mlango wa Mungu, lakini lilizaa chuki kubwa katika familia hata leo hii chuki
hii inaendelea kati ya Waarabu na Waisrael.
Kila mtu anamlango wake kulingana na kifurushi cha
jaribu analopitia. Mlango wa jaribu langu, unaweza usiwe ni njia ya kukutoa
wewe katika jaribu lako, hata kama sote tunapitia katika matatizo au hali sawa.
Jifunze kumsiilza Mungu na kungoja ruhusa yake kwa kila njia anayoifungua mbele
yako
4.
Maneno unayozungumza ndani ya
jaribu/tatizo na mara baada ya kutoka katika jaribu yanatafsiri wewe ni nani na
moyo wako mbele za Mungu.
Katika sura
ya 10 mstari wa 1 wa Wakorintho wa 2, Paul anaeleza ni kwa namna gani Mungu
aliliongoza Taifa la Israel nyakati zote kutoka Misri hadi kuelekea Kanani, na
ni kwa namna gani walianguka katika ibada za sanamu wakiwa njiani, kwakuwa tuu
hawakuona Mungu kama anampango nao na wakamlaumu hata Musa kwa kuwatoa Misri.
Ukiwa ndani
ya jaribu, unaongea nini kuhusiana na wewe mwenyewe? Unaongea nini uhusiana na
Mungu? Unaongea nini kuhusiana na watu ambao wapo kwenye hali kama yako, au
wamekuzidi, au wamepungua kuliko wewe? Chochote unachowaza na kuzungumza juu ya
mabo hayo kitatafsiri ushindi wako na kitakutafsiri mbele za Mungu pia.
Ayubu siku
zote aliishi na mke wake na hakuwahi pengine kujua kuwa mke wake ni mpumbavu
kama wanawake wengine, hadi kipindi ambacho Ayubu alipitia magumu, na Mke wake
akataka Ayubu aongee vibaya kuhusu Mungu. Ashukuriwe Mungu neno kuu moja ambalo
Ayubu alikuwa akizungumza ni “Ninajua
mtetezi wangu yu hai”
Hivyo tatizo
au jaribu lolote linalokukuta, sio geni ni kitu ambacho kama hakikutokea katika
namna ya mifano kutoka kwa wazazi wetu walioishi kabla yetu, basi kitatokea
katika namna ya mfano kwa kizazi kijacho mbele yako. Kwamba kizazi kijacho
kitatakiwa kujifunza namna ulivyomtumaini Mungu katika hilo unalopitishwa na namna ulivyotoka. Na
lengo la Mungu, sio kukutoa katika jaribu au shida na akakulinda usiingie katika
hali hiyo tena.. lakini lengo lake ni kutengeneza nguvu na ustahimilivu ndani
yako, vitakavyo amua na kukupa ushindi kila mara ukutanapo na jaribu au hali
ngumu zaidi.
Umebarikiwa,
SHALOM!!
©Pastor Sam
Gripper
TOTAL
TRANSFORMATION YOUTH MINISTRY/TAG PENUEL LUHANGA
0657670972
No comments:
Post a Comment