SHUKRANI
By Pastor Sam Gripper
18th Feb 2018
Marko 11:24
“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo
mkisali aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
Tunaanza kwa
andiko hili ambalo ndilo hasa linafunua msingi wa shukrani. Pengine hatukuwahi
kuona au hatuwezi kuona uhusiano uliopo kati ya mambo haya matatu, imani, maombi na shukrani. Na huenda
katika somo hili, nikaegemea sana katika haya mawili ya kwanza kuliko katika
shukrani yenyewe maana hayo ndiyo hasa hujenga msingi wa shukrani.
Kitabu cha
Marko hapo juu kinaonesha msingi wa kupokea kitu kuwa haupo katika kuwa na kile
kitu tayari kama majibu ya maombi, lakini upo katika kuanza kukimiliki kile
kitu kabla hata hakijadhihirika kama jibu la maombi yako. Hivyo unapoenda
kumuomba Mungu juu ya kitu ambacho ni hitaji lako, lazima uamini kuwa hicho
kitu umekipokea tayari. Ukilijua hilo, utaepuka kuomba maombi ya lawama, badala
yake utamshukuru maana katika namna ya Imani, tayari unayo majibu ya unachoenda
kuomba.
Na hapo
ndipo mahali ambapo shukrani, imani na maombi hukutana na mambo haya matatu yote
hutegemeana. Tunaomba ili tupate mahitaji yetu, na mahitaji yote tunayoomba au
hata tusiyo yaomba huwa tunayapokea kulingana na kiasi gani tumeamini kuwa mambo
hayo ni yetu tayari. Hii imani hutupa nguvu ya kumiliki na kushukuru sio tuu
kwa yale yaliyodhihirika kwetu, lakini juu hata ya yale ambayo bado
hayajadhihirika na tunamuamini Mungu kuwa yatadhihirika.
Waebrania 11:5-6
“Kwa imani Henoko
alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu
alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza
Mungu.
Lakini pasipo Imani
haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini yeye yuko
na huwapa thawabu wale wamtafutao.”
Katika
andiko hilo hapo juu, yapo mambo ambayo nataka tuyaone lakini zaidi namuomba
Mungu uamini na mimi juu ya mambo hayo. Maandiko yanaanza kueleza katika kitabu
cha Mwanzo 5:22 kuwa, “Henoko akaenda
pamoja na Mungu, naye akatoweka maana Mungu alimtwaa.” Katika kitabu cha
Waebrania hapo juu, maandiko yanatufunulia nini ambacho Mwanzo haikutufunulia
kwa upana.
Maandiko
yanaanza kusema, “kwa imani Henoko
alihamishwa”. Hivyo namna pekee ambayo Henoko aliweza kuishi na Mungu na
kutembea naye, ilikuwa ni namna ya kuanza kwanza kumuamini. Nataka niamini kuwa
maandiko hayamaanishi kuwa Henoko alitembea na Mungu kama mtu awezavyo
kushikana mkono na jirani yake kisha wakatembea. Bali, kutembea na Mungu hapa,
ni kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Nataka
niamini pia kuwa imani ya Henoko ilimpeleka katika point ya kuwa na njia zake binafsi
za kumruhusu Mungu ajidhihirishe kwake, jambo lililomfanya pia Mungu
ajiridhishe kwa Henoko kitofauti sana kiasi cha yeye Mungu kuamua kumchukua
kinyume na utaratibu wa kifo aliouweka baada ya anguko.
Kwakuwa kila
siku, Henoko alikuwa na njia binafsi (tofauti na watu wengine) na thabiti
zilizomfanya Mungu adhihirike kwake, maana yake aliruhusu akili yake imuone
Mungu akiwa halisi katika kila eneo la maisha yake. Na kwa namna hii nataka
niamini kuwa hata namna yake ya maombi na mtazamo juu ya mambo mbalimbali
haikuwa ya kawaida.
Ni rahisi
sana kumshukuru Mungu kama utakuwa umeiruhusu akili yako imuone Mungu akiwa
halisi kwako kila siku na katika kila jambo. Hata maombi yako hayatakuwa ya
lawama badala yake ya kushukuru maana umeruhusu imani ikupeleke mahali flani
pakubwa na muhimu sana pa kumuona Mungu akiwa halisi katika kila jambo.
Ebrania 11:11
Kwa imani hata Sara
mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake kwakuwa
alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu”
Ebrania 11:17, 19
“Kwa imani Ibrahim
alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi
alikuwa akimtoa mwanawe mzaliwa pekee
Akihesabu ya kuwa Mungu
aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena tuko huko kwa mfano.
Wakati ambao
Sara alipokea uwezo wa kupata ujauzito, haukuwa wakati ambao tayari yu
mjamzito. Ulikuwa ni ule wakati ambao alikuwa katika hali ya kushindwa kuwa mjamzito.
Lakini kwa njia ya imani alianza kumiliki jibu la maombi yake katika hali ya
upungufu aliokuwa nao. Hii yote ilikuwa ni kwasababu aliamua kumuona Mungu yu
mwaminifu (mkweli kwa jina lake na kwa ahadi yake mwenyewe).
Ni point
gani hasa ambayo unaanza kumshukuru Mungu? Unamshukuru Mungu mara baada ya kuwa
na muujiza wako mkononi au unashukuru Mungu wakati ambao hata dalili ya kuwa na
muujiza wako haipo? Asilimia kubwa ya watu wanaotoa sadaka ya shukrani katika
makanisa, huwa wanatoa mara baada ya kupokea waliyokuwa wanatarajia, jambo
ambalo sio baya. Lakini lazima tukubali imani yetu ituchukue na kutupeleka
katika point ya kuweza kumshukuru Mungu hata kabla tunayotarajia
hayajadhihirika katika namna ya mwili.
Ibrahim,
alitoa karibia maisha yake yote kuisubiri ahadi ya kumpata Isaka. Lakini mara
baada ya kumpata, anatakiwa afanye maamuzi ya dakika isiyozidi moja kutimiza
juu ya agizo ambalo Mungu alimpa. Katika Ebrania 11:11 tumeona kuwa Sarai
alipokea uwezo wa kupata mimba kabla hajawa na huo uwezo, kwakuwa alimhesabu Mungu kuwa ni mwaminifu. Hapa Ibrahim hasiti kumtoa
Isaka kama sadaka, maana alimhesabu
Mungu kuwa anaweza kumfufua tena.
Hii haina
tofauti na kwa Henoko. Alikuwa na nja zake binafsi ambazo kupitia alimuona
Mungu akidhihirika katika namna kubwa katika maisha yake. Ibrahim alipokuwa
akimtoa Isaka, ndani kabisa ya fahamu zake za kiimani aliamua kumpokea tena
Isaka kama mfano (he received him in a figure). Hivyo alikuwa tayari kumpoteza
Isaka katika mwili ili arudi kummiliki tena katika mfano kama alivyokuwa
akifanya wakati anasubiri ahadi ya kuwa na Isaka itimizwe.
Mtu mwenye
macho na misuli ya namna hii ya imani neno shukrani kwake huwa ni zaidi ya
kusema asante.
Unahesabu
nini/unamhesabuje Mungu:-
¨ Mungu anaporuhusu upite katika
nyakati ngumu ambazo unapoteza kila ulichonacho?
¨ Unapotoa nguvu yako kubwa katika
kuomba na kuamini juu ya hitaji lako, na majibu yakawa tofauti na ulivyotamani
wewe kwa akili zako?
¨ Unapokuwa umepata ahadi kinyume na
ulizo tarajia?
¨ Unapokuwa umepata kila unachotarajia?
Zaburi 100:4-5
“Ingieni malangoni
mwake kwa kushukuru; nyuani mwake kwa kusifu, Mshukuruni lihiidini jina lake;
kwakuwa Bwana ndiye mwema, Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na
vizazi”
Katika kila
hali na kila jambo tunalopitia, lazima tufahamu kuwa halimbadilishi Mungu. Na
tunatakiwa kumshukuru pasipo kujali lolote tunalopita kwasababu hata katika
madhaifu yetu shida zetu, vifungo, kupungukiwa au chochote yeye bado ni Mungu.
Na namna pekee ya kusogelea mahali alipo ni kuamini kuwa yeye yupo (Waebrania
11:6) na kushukuru kama ambavyo Zaburi imezungumza.
©Pastor Sam
Gripper
TAG PENUEL
LUHANGA & TOTAL TRANSFORMATION
0657670972
No comments:
Post a Comment