WITO WA MUNGU - GOD'S CALLING

WITO WA MUNGU
GOD’S CALLING
PASTOR SAM GRIPPER
11th Feb 2018
UTANGULIZI
Tuliumbwa kwa kusudi ili tuweze kulitimiza kusudi. Na kama namna ya kutimiza kusudi la kuumbwa kwetu Mungu hutupa njia za namna ya kuenenda katika kusudi ili kulitimiza.
“Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemuumba kwaajili ya utukufu wangu, mimi nimwemumba, naam nimemfanya”
ISAYA 43:7
Hivyo, kusudi kuu ni kumtukuza Mungu. Na namna kuu ya kuliishi na kulitimiza kusudi hilo ni kwa njia ya kuutumikia WITO WA MUNGU. Huwezi kufikia utimilifu wa kusudi la Mungu pasipo kutembea ndani ya wito. Kusudi ni hatma (destination) na wito ni barabara kuelekea hatma. Wote tunalokusudi moja (kumtukuza Mungu kupitia maisha yetu), lakini njia za kulifikia kusudi hilo (Wito) huweza kuwa tofauti.
“Ndani yake tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa (tukiitwa) tangu awali, sawasawa na kusudi lake”
EFESO 1:11
KUSUDI - > WITO - > HUDUMA - > KARAMA/VIPAWA/VIPAJI
Kwa mujibu wa Waefeso 1:11, ni wazi kuwa kuitwa kwetu ni kwasababu ya kusudi ambalo tunatakiwa kulitimiza. Na mfululio huo hapo juu, unaoesha kuwa ili tuweze kufikia Kusudi tunahitaji Wito na Wito unatimizwa kupitia Huduma na Huduma hutimizwa kwa kuvitumia vipaji, karama na vipawa.
Anaandika Pastor Jimmy & Caroline Murphy katika kitabu chake cha Manabii na unabii katika kanisa la leo, sura ya 6 kuwa huduma na karama au vipaji, ni sawa na fundi seremala na box lake la vitendea kazi. Fundi seremala ni mhudumu anayetoa huduma, lakini huduma yake haiwezi kulifikia kusudi husika, pasipo matumizi ya zana za kazi ambazo ni karama, vipawa na vipaji.

Kama lipo kosa ambalo vijana wengi, nikiwemo na mimi hulifanya, ni kudhani kuwa kila mahali Mungu anapokuita (anapodhihirisha wito wake kwako), ni kwamba anakupeleka katika kutumika katika zile huduma za ualimu, unabii, uchungaji nk. Jambo ambalo wengi ndio hutafsiri kuwa ni maana ya wito.
 Lakini nina uhakika kuwa Mungu anaweza akakuita na kukupaka mafuta pia kumtumikia kwa kipaji ulicho nacho. Uchoraji, uchongaji, ususi, upambaji, uandishi, uigizaji nk. Mungu alipomuumba Adam na kumuweka katika bustani ya Edeni, alitegeea Adam atumike sio kama mchungaji, mwanamaombi , nabii au muinjilisti, lakini alitakiwa kutumika kama Mkulima.
Hivyo wito wa Mungu ka mtu ni mpana tofauti na wengi tulivyokuwa tunadhani ma ana lengo la wito wa Mungu kwa mtu, ni kumleta mtu katika point ambayo atatumia yote aliyonayo (vipaji na karama) ili kulitimiza kusudi la kuumbwa kwake ambalo ni kumtukuza Mungu.
MAANA YA WITO
Neno Wito linatokana na tendo kuita au kutamka jina. Na kimsingi kutamka jina (to name) ni zaidi ya kukitambua kitu (identifying/labeling). Kutamka jina ni kukifanya kitu kiwe (to call something into being/ to make).
“Mungu akasema iwe nuru, ikawa nuru. Akaiita nuru mchana na giza akaliita usiku”
MWANZO 1:3
“Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje, kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake.”
MWANZO 2:19
Maandiko haya mawili, yanaweza yakanisaidia sana kuielezea tofauti iliopo kati ya kuita na kukitambua kitu. Mwanzo 1:3, inaonesha jambo ambalo kimsingi ndiyo msingi wa kuitwa kwetu. Nuru haikuwepo hapo awali. Lakini Mungu anaifanya nuru iwe kwa kuiita. Hivyo nuru inatokea katika hali ya utupu na inakuwa dhahiri kwakuwa tuu Mungu ameiita.
Mwanzo 2:19, Mungu anaviumba viumbe, ndege na wanyama ambao kimsingi havikuwepo na kuvileta katika hali ya kuwa, na baada ya kuwa anampa Adamu kazi ya kuvitambua (identifying/labeling) viumbe hivi kwa majina.
Hivyo msingi wa wito ambao Mungu anatuita, ni kuitwa kutoka katika hali ya upweke na utupu na kuletwa katika hali ya kuwa ili tulifikie kusudi lake. Ni katika hali hii Mugu huwa anatuita sio kwaajili ya kutumia tuu tulivyo navyo, lakini zaidi kuviumba vitu vipya ndani yetu ili tuvitumie kwaajili ya kazi yake.
AINA KUU 2 ZA WITO
1.     Wito ambao wanadamu sote tumeitiwa, kuwa wabeba sura ya Mungu
Kama tulivyotangulia kuangalia hapo juu, kuwa msingi wa kwanza wa wito wetu ni kuletwa katika hali ya kuwa (being) na aliyetuita ambaye ni muubaji wetu (Mungu). Na ndio hasa jambo muhimu ambalo Isaya amelizungumza katika Isaya 43:7 kwamba tumeumbwa na kuitwa ili kulitimiza kusudi la Muumba.
Tumeumbwa (tumeitwa) ili kumuakisi muumba katika maisha tutakayoyaishi na kupitia maisha hayo, tutafikia kusudi kuu la kuumbwa kwetu ambalo ni kumtukuza Mungu. Tunatakiwa kuishi kwa kumuakisi Mungu kwakuwa, sura ya Mungu kwa mtu sio physical structure lakini ni spiritual structure.
Sura ya Mungu kwa mtu, ni uwakilishi (divine presentation) anaokirimiwa mwanadamu ili kumwakilisha Mungu katika maisha yake yote ya ulimwengu wa mwili.
MAMBO MAKUU 5 YANAYOELEZA SURA YA MUNGU KWA MTU
a.       Asili ya mwanadamu
Mwanadamu ni muunganiko wa roho na mwili jambo linalompa maisha katika ulimwengu wa roho na mwili pia. Katika ulimwengu wa roho, anachukua asili ya Mungu (Yohana 4:24), katika ulimwengu wa mwili anaishi kama balozi na hekalu la Mungu  (1KOR 6:19)
b.      Utashi na dhamiri
Utashi ni uwezo lakini zaidi uhuru wa kufanya machaguo na maamuzi mbalimbali. Hii ndio sababu ambayo ilifanya kwamba pamoja na Mungu kujua kuwa Adamu atakuja kumkosea, lakini bado hakumzuia juu ya jambo hilo mbele yake, maana alimkirimia utashi.
Lakini pia utashi ni uwezo wa kupima matokeo  kabla ya kuchukua hatua ya kulitenda jambo. Kama ambavyo Mungu anaweza kuutazama mwisho wa jambo kabla ya mwanzo, ndivyo ambavyo mwanadamu anaweza kupima matokeo ya jambo kabla halijafanyika. Mfanya biashara kabla hajaanza kufanya biashara, huwa anakaa na kuipima kisha anachukua hatua juu ya alichokiona. Kwasababu hii ni tabia ya Mungu ambayo ameiwekeza kama  sura yake kwa mtu.



c.       Dhamiri
Uwezo wa Mungu kuufunua utakatifu wake kwa mtu ili kumfanya tu awe na muitikio sahihi kwa maadili. Mungu anamuumbia mtu dhamiri ili imuongoze katika maamuzi na machaguo anayoyafanya na kumleta mtu katika point ya kuwa mtakatifu kama yeye Mungu alivyo mtakatifu.
d.      Uwezo wa kuumba (Ubunifu)
Kila tunapofanya kazi ya uundaji, tunaakisi uungu wa Mungu. Hivyo hii ni sura ya Mungu aliyoiwekeza kwa mtu
e.       Uwezo wa kuhusiana
“Kila mmoja kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu”
1PETRO 4:10
Hili ni jambo lingine ambalo linaelezea sura ya Mungu kwa mtu. Uwezo wa kuhusiana, unafanya vipawa na karama ziwe rahisi kuhudumiana na kufaidishana. Kati ya mambo yote mema ambayo Mungu aliyafanya katika bustani ya Edeni, ni jambo moja tuu halikuwa jema machoni pake yeye mwenyewe.
 Na jambo hili ni mtu kuwa peke yake. Sura ya Mungu kwa mtu ni upendo, na ndio maana huwezi ukampenda Mungu usiyemuona wakati mtu unayetakiwa kuhusiana naye hujampenda.
Hivyo, wito wetu wa kwanza ni kuwa wmeba sura na mfano wa Mungu, jambo ambalo kila aliyeitwa na Mungu (kutoka hali ya ktokuwepo na kuletwa hali ya kuwa) anaushiriki.
2.     Wito ambao unawahusu wateule
“Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”
MATHAYO 22:14
Aina hii ya pili ya wito ni msingi wa maisha ya mwamini ambayo yana tokana na mwitikio wa kazi ambayo Mungu ameiweka ndani yake. Ni kweli, sote tumeitwa, kwa maana ya kuumbwa kutoka katika utupu hadi kuwa hivi tulivyo, lakini si kweli kwamba sote tumeteuliwa kuifanya kazi ambayo Mungu ameikusudia kwa wito wetu wa pili.

“Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.”
YOHANA 1:11-12
Hivyo, wito wetu mkuu kama familia inayoshiriki neema ya wokovu wa Mungu, ni kurejesha sura ya Mungu kwa mtu iliyopotezwa kwa sababu ya uovu
“Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu, kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakao waondolea dhambi, wameondolewa, na wowote mtakao wafungia dhambi, wamefungiwa”
YOHANA 20:21-23
Kama Mungu alivyofanya katika Mwanzo 2:7 kupuliza pumzi yake ya uhai puani mwa mwanadamu mara baada ya kumuita, ndivyo ambavyo Yesu anafanya katika andiko hili. Mara baada ya kufufuka, anawaumba wanafunzi wake kwa upya na kuwatiisha katika mamlaka ya utawala kama Makristo hapa duniani. Anawapulizia pumzi yake ya uhai, na kupitia pimzi hiyo anawapa Roho Mtakatifu (anafanya uumbaji wa pili) na kuwapa mamlaka ya kusamehe kwa niaba ya Mungu.
Huu ni wito wetu wa pili ambao tumeitiwa. Mara baada ya anguko la mwanadamu, sura ya Mungu kwake ilifutika na kuliathiri kusudi la Mungu kwake. Hivyo mwanadamu katika kutenda, akawa hawezi tena kutenda kwa kutegemea utashi na ufahamu wake ili kumpendeza Mungu kama ilivyokusudi la kuumbwa kwake. Hivyo kwa nana yoyote, lazima sura ya Mungu kwa mtu irejeshwe. Na Roho Mtakatifu kupitia sisi, ndio anaifanya hiyo kazi kila mara tunapowafikia watu walio gizani.
“Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake. Wala hawezi kutenda dhambi kwasababu amezaliwa kutokana na Mungu.” Katika hili, watoto wa Mungu ni dhahiri na watoto wa ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake”
1YOHANA 3:9-10
Hii ndio kazi ya pili  tuliyoitiwa ili kuwafanya watu wasiomjua Mungu warudi katika kuwa wabeba sura ya Mungu. Hili halihitaji uwe muhubiri, mwimbaji, muinjilisti, mwalimu nk. Hizo ni huduma tuu za kuuishi na kuutimiza wito kama ambavyo unaweza kuwa muuza nyanya na kupitia kazi yako, watu wakaokolewa.


“Vivyo hivyo, nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”
MATHAYO 5:16
ILI KUTAMBUA WITO NA POSITION AMBAYO UNATAKIWA KUWA ILI KUUTUMIKIA WITO WAKO UNATAKIWA KUFANYAJE?
Hili ni swali ambalo rafiki yangu mmoja aliwahi kuniuliza. “Nawezaje kuutambua wito wangu au mahali ambapo natakiwa nisimame ili kuutimiza? Natakiwa kwanza niwe mchungaji ili kuutimiza au?”
Kama nilivyotangulia kuandika hapo awali. Watu wengi na mimi nikiwepo, tumekuwa tukilichukia sana hili neno wito wa Mungu kwakuwa, tumewaza kuwa kila mara Mungu anapofunua wito wake kwetu, ni lazima atuchukue na kutupeleka katika uchungaji, uinjilisti, ualimu nk hata kama hatupendi. Nakubali na ninayatambua mazingira ambayo Mungu aliwahi kuwaita watu katika maeneo nyeti sana ya kiutumishi hata kama hawakupenda kutumika huko. Lakini ni kwa makusudi na nyakati maalu, Sio mara zote Mungu hufanya hivyo.
Unahitaji kuwa na Roho Mtakatifu
“Yeye atanitukuza mimi; kwakuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”
YOHANA 16:14
Roho kwa kuyatwaa yaliyo ya Mungu na kutupasha habari, huzifanya upya fahamu zetu ili tuyajue mapenzi ya Mungu kwetu ni yapi. Tendo la kuyajua mapenzi ya Mungu hutupa muitikio sahihi juu ya nini Mungu anataka tufanye.  Hili hutusaidia kukaa katika position ambayo yeye Mungu amekusudia kwaajili ya kutuwezesha kutembea ndani ya wito huu mkuu tulio teuliwa kuufanya.
Roho ndio hutoa karama na vipaji na humassign mtu mahali ambapo yeye Roho ameona mtu huyo tafaa kuwepo hapo. Hivyo, pasipo Roho Mtakatifu, ni ngumu sana kujua ni wapi unatakiwa kukaa ili kuutimiza wito wako. Roho Mtakatifu yupo tayari kukusaidia, unachotakiwa kufanya ni kuwa tayari kumpoea na kuruhusu badiliko kamili ndani yako.
1 WAKORINTO 12:28, WAEFESO 4:11, WARUMI 12:6-8
Mara baada ya kujua karama na kipawa chako, hakikisha huchi kukichochea. Tumia mara nyingi kadri uwezavyo pasipo kujali lolote. Hiyo ni namna ya wito ulioitiwa na utadaiwa kama utashindwa kutenda kwa bidii.
BE TRANSFORMED!


©By Pastor Sam Gripper
    TAG PENUEL LUHANGA & TOTAL TRANSFORMATION YOUTH MINISTRY
    0657670972

Unknown
Unknown

This is a short biography of the post author. Maecenas nec odio et ante tincidunt tempus donec vitae sapien ut libero venenatis faucibus nullam quis ante maecenas nec odio et ante tincidunt tempus donec.

No comments:

Post a Comment